Si jambo rahisi sana kuweka akiba kila siku kutoka katika sehemu ya kipato chako na usiitumie kabla ya wakati wake na nje ya malengo yake. Kuweka akiba kunahitaji nidhamu ya hali ya juu pamoja na kuwa na kiasi (yaani, uwezo wa kujizuia na kujitawala). Kama huna nidhamu ya fedha na huna kiasi (self-control) huwezi kuweka akiba; utaiweka leo na kesho utaitumia kabla ya kufikia kiasi ambacho ulikuwa unakihitaji ili kutimiza lengo fulani katika maisha yako. Akiba ni kitu kilichotengwa na kuhifadhiwa vizuri na katika hali ya usalama kwa ajili ya matumizi muhimu au manufaa ya baadaye. Akiba ni njia ambayo mtu anaweza kuitumia kujikusanyia mali au fedha kwa ajili ya kutimiza malengo yake ya baadaye au kwa ajili ya manufaa yo yote katika siku za usoni. Kwa hiyo kuweka akiba ni jambo la muhimu sana katika maisha ya mtu ye yote mwenye hatima. MBINU ZITAKAZOKUWEZESHA KUWEKA AKIBA NA IKADUMU AU IKAKAA Zifuatazo ni mbinu zitakazokusaidia kuweka akiba yako na ikakaa au kudumu mpaka itakapofika wakati wake wa kuitumia ambao umekusudia; 1. Weka malengo katika maisha yako na udhamirie kuyatimiza. Malengo ni mambo ambayo unatamani uyafikie katika maisha yako, ni makusudio yako ya siku za usoni yanayolenga kuboresha maisha yako na ya wengine pia. Kama utakuwa na malengo basi utaona umuhimu wa kuyatimiza, na kama utaona umuhimu wa kuyatimiza basi utaona ulazima wa kuweka akiba. Hautatumia nguvu nyingi kuweka akiba kwa sababu utajijengea nidhamu ya matumizi yako ya fedha hasa unapokuwa umedhamiria kwa moyo wako kutimiza malengo yako. Pasipo malengo na mikakati ya kutimiza malengo hayo, fedha hupotea kupitia kitu chochote kwa matumizi yasiyokuwa ya lazima. Ili kuweka malengo ni lazima uwe ni mtu unaejiangalia kwa jicho la kesho na kutengeneza picha ya namna gani unataka kuwa kesho; usijiwazie mambo madogo, jiwazie mambo makubwa, na usijiwazie wewe mwenyewe bali ujiwazie katika kugusa jamii ya watu wanaokuzunguka. Kama huna muda wa kufikiri kesho yako, na kama huna muda wa kufikiri mwisho wako, daima huwezi kuweka malengo yo yote. Malengo yako yaambatane na mpango mkakati wa kuyatimiza, na sehemu ya mpango huo iwe ni akiba utakayokuwa anaweka kidogo kidogo kwa kadili unavyopata fedha. Usiishi bila malengo na usiwe na malengo bila mpango mkakati wa kutimiza malengo hayo. Muhubiri 3:1 Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu Hakikisha unakuwa na kusudi (lengo) katika kila kipindi cha wakati ulionao chini ya jua kwa sababu wakati upo kwa ajili ya kutimiza kusudi au lengo katika maisha yako. Usikae kae tu bila malengo kwa sababu utimilifu wa maono aliyonayo mtu ni mkusanyiko wa malengo yaliyotimia aliyonayo mtu kuelekea maono aliyonayo mtu huyo. 2. Dhamiria kwa moyo wote na shahuku yote kuweka akiba ili kutimiza malengo yako na maono yako. Kama unayo malengo ambayo umeyaweka vizuri na wazi kwako, basi kinachofuata ni kuandaa mikakati ya kufikia malengo hayo; na kama ni malengo yanayohitaji fedha, basi mkakati mmoja wapo wa kufikia hayo malengo ni wewe kuanza kuweka fedha kidogo kidogo kama akiba itakayokuwezesha kutimiza malengo yako. 1 Nyakati 22:3, 5, 14 [3] Daudi akaweka akiba tele ya chuma kwa misumari ya tarabe za malango, na kwa mafungo; na ya shaba akiba tele isiyo na uzani; [5] Daudi akasema, Sulemani akali mchanga bado, na mwororo, nayo nyumba atakayojengewa Bwana haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa. [14] Basi sasa, tazama, katika shida yangu, nimeiwekea akiba nyumba ya Bwana, talanta elfu mia za dhahabu, na talanta elfu elfu za fedha; na shaba na chuma isiyo na uzani; kwa vile zilivyo tele; miti tena na mawe nimeweka akiba, nawe utaweza kuongeza. Akiba anayozungumza hapa Daudi hakuiweka ndani ya kipindi kifupi cha muda, ulikuwa ni mkakati wake siku chache tu baada ya kuingia katika ufalme wake alipokuwa na lengo la kumjengea Mungu nyumba ya kuabudia. Alianza kuweka kidogo kidogo, na wakati huu alipokuwa anazungumza akiba ilikuwa na thamani kubwa sana isiyoweza hesabika. Thamani ya akiba haipimwi katika kiwango unachoweka kuwa akiba sasa hivi au leo, thamani ya akiba inapimwa katika uwezo wake wa kutatua changamoto zako za kesho na si leo. Kiasi unachoweka leo kinaweza kisiwe kina thamani ya kujibu changamoto yo yote sasa lakini kinapokutana na kiasi kingine utakachoweka kila upatapo kitakuwa na thamani kubwa kiasi cha kujibu changamoto zako zote za kesho. Kama huna malengo na huna mkakati wa kutimiza malengo yako, kuweka akiba kwako itakuwa ni swala gumu sana. Wakati mwingine kujenga nyumba, au kuanzisha biashara fulani au kununua kiwanja inaweza kuwa ngumu kwa sababu ya gharama kuwa kubwa; unaweza usifanye leo lakini ukakusudia kufanya kesho, na kama umekusudia basi weka makakti utakaokupunguzia gharama ifikapo kesho, anza kuweka akiba sasa. Kiasi kidogo kidogo unachoweka leo ambacho hakiwezi kujenga nyuma, kesho kitakapokuwa kimekutana ni kiasi kingine ulichokuwa unaweka kidogo kidogo kitakuwa na thamani ya kujenga nyumba. Kwa hiyo dhamiria kuweka akiba. 3. Kuwa na bajeti ya pato lako la sasa hivi ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima katika maisha yako ya kila siku. Bajeti ni makadirio ya mapato na matumizi ya pato lako katika kipindi fulani cha muda. Bajeti ndiyo inayoamua mapato yako yatumikeje, fedha yako ielekee wapi na kwa kusudi gani. Kama huna bajeti fedha yako itatumika pasipo utaratibu kwa vitu visivyo na maana na visivyotimiza malengo yako hata kidogo. Bajeti ndiyo inayokujengea nidhamu ya matumizi yako ya fedha iwapo fedha yote unayoipata utakuwa umeitengenezea bajeti inayojibu uhitaji wako wa sasa na ule uhitaji wako wa baadaye. Kama mipango yako yote utaitengenezea bajeti pato lako lote litakapokuja litaingia na kugawanywa katika bajeti uliyonayo bila ya kupoteza cho chote. Sasa basi, akiba iwe ni sehemu ya bajeti yako, yaani kuwepo na kiasi cha fedha katika bajeti yako inayoelekezwa kwenye akiba yako. Kama akiba yako haitakuwa ni sehemu ya bajeti yako na badala yake ukawa unasubiri mpaka fedha ibaki ndipo uweke akiba, akiba kwako itakuwa ni ndoto za bunuwasi. 1 Nyakati 29:2 [2] Basi kwa uwezo wangu wote nimeiwekea akiba nyumba ya Mungu wangu, dhahabu kwa vitu vya dhahabu, na fedha kwa vitu vya fedha, na shaba kwa vitu vya shaba, na chuma kwa vitu vya chuma, na miti kwa vitu vya miti, ; vito vya shohamu, na vya kujazia, vito vya njumu, na vya rangi mbalimbali, na mawe ya thamani ya kila namna, na marimari tele. Maandiko haya yanaonyesha mchanganuo wa bajeti aliokuwa nao Daudi juu ya nyumba ya Mungu na kwa kufuata ile bajeti akaiwekea akiba nyumba ya Bwana Mungu. Bajeti ni kichocheo cha wewe kuweka akiba yako na kuilinda hata ifikie malengo yake ya kuwekwa. Kama hautakuwa na bajeti huwezi kuwa na msukumo wa kuweka akiba hata kidogo, na hata kama utaiweka, kesho au baadaye utaitumia tu kwa sababu hautaona haja ya hiyo akiba kuendelea kuwepo. Jambo la muhimu hapa ni wewe kuhakikisha bajeti yako inatosha katika mahitaji ya muhimu ya kila siku ndani ya muda ambao unapata kipato chako, kama ni kwa mwezi, au kwa wiki, au kwa siku. Sasa hii ni pamoja na wewe kupunguza mambo au matumizi yote yasiyo ya lazima ili kuhakikisha fedha yako inatosha bajeti yako yote katika muda huo. Daima usipange bajeti kubwa inayozidi uwezo wa kipato chako, panga bajeti kulingana na kipato chako. 4. Tambua na uone uhitaji wako wa kesho na haja ya kuanza mkakati wa kuutimiza sasa kwa kuweka kiasi kidogo kidogo kama akiba ikiwa ni sehemu ya bajeti yako ya kila siku katika pato lako la sasa. Kama hutaweza kuona uhitaji wa kesho na umuhimu au ulazima wake daima huwezi kuwa na msukumo wa kuweka akiba kwa sababu hutaona ulazima na sababu ya kuweka akiba hiyo. Unajiandaa vipi kukabiliana nachangamoto za kesho zitakazokuwa zikikukabiri wewe au familia yako? Mwanzo 41:35, 36 [35] Na wakusanye chakula chote cha miaka hii ya myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika mji. [36] Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa. Unajua unaweza kufa kwa sababu ya kukosa matibabu sahihi ambayo yalihitaji fedha ambazo hukuwa nazo kwa wakati zilipokuwa zikihitajika. Mtu mwenye hekima huwekeza hata kwa ajili ya afya yake. Sasa wewe unajiandaaje kwa ajili ya hitaji la baadaye la matibabu, au ya kwako mwenyewe au ya mke/mume wako au ya watoto wako? Unajiandaaje na uhitaji wa ada ya shule ya watoto wako siku ya kesho? Ukiona uhitaji wa kesho utakuwa na msukumo wa kuweka akiba. Chakula kilichokusanywa na Yusufu kilikusanywa kidogo kidogo kwa muda wa miaka saba hata kikafikia kiasi ambacho hakikuweza kuhesabika, na mwisho wa siku kilijibu uhitaji wa njaa katika miaka ile saba ya njaa. Kuweka akiba pia ni sehemu ya kuishi kwa imani; kuishi kwa imani ni pamoja na kuino kesho yako na uhitaji wake na kisha ukajiandaa kwa ajili ya kesho hiyo. Sasa wewe kuwa mjinga kwa kubaki unasema kuwa unaishi kwa imani na mambo ya kesho yatajisumbukia; mimi nakusubiri nikuone hiyo kesho wakati mambo hayo yanajisumbukia. Badala ya mambo kujisumbukia utakuwa unayasumbukia hayo mambo pasipo kuwa na msaada. Hakikisha akiba inakuwa ni sehemu ya bajeti yako kulingana na kipato unachopata; na ukitaka kufaulu hakikisha kuwa ni kiasi kidogo ukilinganisha na kile kinachobaki ili kukidhi uhitaji wako wa kila siku. Ukiweka akiba kubwa na mfukoni ukaishiwa, lazima utarudi tena na kuichukua hiyo akiba na kisha kuitumia kwa mahitaji yako ya kila siku. 5. Ilinde akiba hiyo, usiitumie nje ya malengo, itegemee tu kwa ajili ya malengo yake na si vinginevyo. Akiba hulindwa ili isitumike nje ya malengo kwa sababu huwa kuna shida na uhitaji unaojitokeza hapo katikati na wakati mwingine unaweza usiwe wa lazima. Sasa kama hutailinda akiba yako kwa kuwa na nidhamu ya hali ya juu na uwezo wa kujitawala na kujizuia katika matumizi yako ya fedha ya kila siku, utajikuta unaitumia tu hiyo akiba. Mwanzo 41:35, 36 [35] Na wakusanye chakula chote cha miaka hii ya myema ijayo, wakaweke akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinde kuwa chakula katika mji. Baada ya makusanyo, na baada ya kutoa kiasi cha makusanyo na kukiweka akiba, inayofuata ni kuilinde hiyo akiba ili isitumiwe kabla ya wakati wake. Miaka saba ya shibe iliwezekana kabisa kutumia kile chakula ambacho walikiweka akiba kabla ya miaka saba ya njaa, lakini Yusufu alikilinda ili kisitumiwe kabla ya wakati. Lakini pia katika miaka ile ya njaa ilipowadia, bado walikilinda kile chakula kilichowekwa akiba ili kisitumiwe vibaya nje ya utaratibu uliokuwa umewekwa ili kitoshe kutimiza uhitaji wote. Kuna uhusiano mkubwa sana kati ya matumizi na uwekaji wa akiba. Kama mtumiaji hatajizuia na kujitawala kwa kujenga nidhamu ya matumizi atajikuta anaitumia akiba ile ile aliyoiweka leo kwa ajili ya kesho. Mkulima hasa yule wa zamani ambaye alipaswa ahifadhi mbegu yeye mwenyewe, alikuwa na nidhamu kubwa sana; mbegu ilikuwa ni bajeti yake ya lazima, aliitenga mapema sana na kuificha mpaka kipindi cha kilimo. Hata kama hapa katikati atapitia changamoto kubwa ya njaa, asingeliweza kula zile mbegu kwa sababu ni akiba ya baadaye. Kwa hiyo, kama huwezi kujizuia kutumia, huwezi kuweka akiba na ikakaa. Na kama huwezi kupanga bajeti yako vizuri, huwezi kuweka akiba na ikakaa. Kama huoni uhitaji wa baadaye na kuwa na mkakati wa kuujibu sasa, bado akiba kwako itakuwa ngumu kuiweka. Ni lazima uwe na dhamira ya dhati, ni muhimu ukawa na malengo madhubuti, na ukakusudia kuilinda akiba yako, ndipo utakapoweka akiba nayo ikakaa. Hakuna mtu ye yote aliyefanikiwa pasipo kuweka akiba. Hata matajiri wote ili wasirudi katika umaskini na badala yake waendelee kuinuka huweka akiba katika hicho wanachokipata, na walianza kuweka akiba wakiwanacho kidogo na ndiyo maana waliongezeka na kufikia malengo yao. Ukitaka uwe maskini na ubaki kuwa maskini ambaye hajatimiza hata moja ya lengo lake, wewe usiweke tu akiba, tumia pato lako lote kwa matumizi ya sasa yasiyokuwa na faida katika kesho yako. Na, Mch. Ezekiel P. Bundala 0673 184 468