"Collabo" ni nini na je mwimbaji wa nyimbo za injili ni sawa kufanya collabo na mwimbaji wa kidunia?

Discussion in 'Maswali na Majibu Kuhusu Biblia na Ukristo' started by Ezekiel P Bundala, Feb 18, 2019.

  1. Ezekiel P Bundala

    Ezekiel P Bundala Unaishi kwa ajili ya Mungu na si kwa ajili yako

    Messages:
    657
    Likes Received:
    215
    Trophy Points:
    43
    Occupation:
    Pastor
    Location:
    Dodoma
    "Collabo" (au Kolabo) ni kifupisho katika lugha ya Kiswahili kisicho rasimi cha neno la Kiingereza "collaboration" ambalo Kiswahili chake halisi ni "ushirikiano." Hili ni neno linalotumika sana katika tasnia ya muziki kwa ujumla wake; ule wa Injili (Gospel music) na ule muziki wa kidunia (secular music).

    Collabo au Kolabo ni hatua au mchakato wa watu au vikundi viwili au zaidi wanapokutana kwa makubaliano maalumu ili kufanya kazi pamoja kwa kusudi la kufanikisha lengo fulani kupitia kazi hiyo wanayoifanya. Katika tasinia ya muziki, collabo inatokea wakati waimbaji au wana-muziki wawili au zaidi wanaofanya kazi kila mmoja peke yake wanapokuja pamoja kwa makubaliano na kufanya kazi pamoja katika wimbo mmoja watakaoimba wote wawili kwa malengo fulani sawasawa na makubaliano yao.

    Collabo katika tasnia ya muziki inaweza kufanyika si kwa waimbaji tu lakini pia kwa waandishi wa nyimbo, watunzi wa melodi, wazalishaji (producers), wapigaji wa muziki (musicians) wanapokuja pamoja ili kufanya kazi pamoja kwa lengo mahususi.

    Malengo Ya Kufanya Collabo
    1. Kuongeza nguvu katika kile mnachokifanya; waimbaji wawili tofauti au zaidi au vikundi viwili tofauti au zaidi wanapokutana pamoja ili kufanya collabo ni ili kuongeza nguvu katika kazi wanayoifanya kwa sababu wawili si kama mmoja aliye peke yake; Biblia inasema, mmoja atafukuza elfu zake lakini wawili watafukuza kumi elfu (Kumbukumbu 32:30); nguvu ninayozungumzia hapa si tu katika ulimwengu wa damu na nyama lakini hasa katika ulimwengu wa roho katika kusababisha matokeo ya ki-Mungu katika maisha ya watu.
    2. Kuongeza uzuri, ubora na mvuto wa kazi: wakati mwingine collabo inafanywa kwa lengo la kuongeza ubora, uzuri na mvuto wa kazi ili iwavutie watu wengi zaidi.
    3. Kuongeza hadhira au mashabiki: Collabo pia hufanyika kwa kusudi la kuongeza watu watakaokuwa wanafuatalia kazi zako. Kwa hiyo lengo lake ni kuunganisha mashabiki wa pande mbili na kuwafanya wote kwa pamoja wawe pia mashabiki wako.
    4. Kutumika pamoja kwa lengo la kuujenga ufalme wa Mungu; na hii wakati mwingine inatokana moja kwa moja na msukumo wa Roho Mtakatifu ndani ya wahusika unaowasukuma kufanya kazi pamoja.
    5. Kuinuana na kutambulishana: Hii hutokea hasa kati ya mwimbaji chipukizi na mwimbaji ambaye tayari ni mkongwe; mwimbaji chipukizi huamua kufanya collabo na mwimbaji mkongwe ili kupitia kazi hiyo aweze kujitamburisha kwa hadhira, na pia mwimbaji mkongwe anaweza kufanya collabo na chipukizi kwa lengo la kumwinua zaidi kihuduma.
    Je, Mwimbaji wa nyimbo za Injili anaweza kufanya collabo na mwimbaji wa nyimbo za kidunia?

    2 Wakorintho 6:14 - 18
    [14] Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?
    [15] Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani na yeye asiyeamini?
    [16] Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
    [17] Kwa hiyo,
    Tokeni kati yao,
    Mkatengwe nao, asema Bwana,
    Msiguse kitu kilicho kichafu,
    Nami nitawakaribisha.

    Kufungiwa nira ni kufungwa katika uhusiano unaowaunganisha kiroho na si tu kimwili na hasa katika mambo yanayohusisha miungu na ibada, ama Mungu wa kweli au mungu wa dunia hii. Collabo na hasa katika mambo ya kiroho yanayohusikana na ibada zinazomwelekea Mungu au miungu moja kwa moja ni kufungiwa nira. Sasa kuna kufungiwa nira ilivyo sawasawa na kufungiwa nira na watu wasioamini kwa jinsi isivyo sawasawa. Je, kufanya kolabo na mtu asiyeamini ni sawa kwa mtu anayeamini katika huduma ya uimbaji?

    SIO SAWA KABISA mtu mwimbaji wa nyimbo za Injili (aliyeokoka) kufanya collabo au kushirikiana na mwimbaji wa nyimbo za kidunia kwa sababu zifuatazo kulingana na nuru ya maandiko matakatifu katika kifungu hapo juu;

    Uimbaji ni Swala linalotuunganisha na Mungu au miungu katika ulimwengu wa roho:
    Uimbaji ni Jukwaa linalotumika kuabudu kwa maana ya kupeleka sifa na shukrani zetu kwa Mungu zilizojaa mioyoni mwetu na katika vinywa vyetu lakini pia kupokea kutoka kwa Mungu na kutoa kwa watu kile tulichopokea kutoka kwa Mungu ili kuujenga ufalme wake.

    Kwa mantiki hii, uimbaji ni maisha ya utumishi kwa Mungu unayemwabudu ndani ya ufalme wake. Waimbaji wa nyimbo za kidunia hupokea kutoka kwa mungu wa dunia hii wakati waimbaji wa nyimbo za injili hupokea kutoka kwa Mungu wa mbinguni; kwa sababu hiyo watu hawa wawili kufanya collabo ni kusababisha vita ya miungu kati ya Mungu wa mbinguni na mungu wa dunia hii; ni kusababisha vita ya falme, kati ya ufalme wa mbinguni na ufalme wa dunia hii kwa sababu HAKUNA ULINGANIFU KATI YA KRISTO NA BELIARI (2 Korintho 6:15).

    Uimbaji ni dhabihu juu ya madhabahu ndani ya hekalu la Mungu, hivyo hapana mapatano kati ya hekalu la Mungu na sanamu:
    Ni muhimu sana tukaelewa kuwa, uimbaji ni jambo ambalo linafanyika madhabahuni, ni dhabihu inayotolewa madhabahuni kumwelekea Mungu, kamwe haiwezi kutolewa katika madhabahu za miungu mingine au pamoja na madhabahu za miungu mingine. Watu waliookoka ni hekalu la Mungu ambalo Roho Mtakatifu anakaa ndani yao na kutembea katikati yao (2 Korintho 6:16); na kwa sababu wao ni hekalu Mungu amewafanya wawe wahudumu wa madhabahuni kwa kuwafanya mahuhani kwa damu ya Yesu Kristo ili wamtolee dhabihu za sifa (Waebrania 13:15; 1 Petro 2:9).

    Kwa upande mwingine watu ambao hawajaokoka nao ni hekalu la sanamu kwa sababu ile roho ya mungu wa dunia hii anaishi ndani yao; kile wanachokifanya ni ibada ya sanamu, ni ibada kwa mungu wao, na uimbaji ni dhabihu wanayoitoa kwa miungu yao hiyo na ndio sababu kila wanachokifanya wanakifanya ili kuupendeza ulimwengu na sio Mungu. Sasa wawili hawa, asiyeamini na aliyeamini kufanya collabo ni kulichafua hekalu la Mungu kwa sanamu.

    Katika nyakati za Israeli, walipokuwa wanaingia ili kuimiliki nchi ya ahadi, Mungu aliwaagiza kwamba, wavunje madhabahu zote za miungu na sanamu zote ili kusiwepo na mvutano kati ya Mungu na miungu na kati ya hekalu la Mungu na sanamu kwa sababu kamwe, hekalu la Mungu na sanamu haviwezi kupatana.

    Biblia inasema kuwa, kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo (Zaburi 33:1), na katika Biblia kila watu walipotaka kumwimbia Mungu walijitakasa ili kusiwepo na mkanganyiko kati ya hekalu la Mungu na sanamu jambo ambalo lingelipelekea ibada zao kukataliwa na Mungu (2 Nyakati 5:11-14).

    Hapana urafiki kati ya haki na uasi wala shirika kati ya nuru na giza
    Watu waliookoka ni wenye haki na pia ni wana wa nuru (1 Wathesalonike 5:5) wakati wasioamini ni wana wa giza na wana wa kuasi (Waefeso 2:2). Kwa sababu hiyo, hakuna uhusiano wala ushirika wo wote wa kihuduma kati ya haki na uasi na kati ya nuru na giza kwa sababu hivi vyote vimepingana tokea kwenye asili yake; huyu ana asili ya haki na nuru na huyu mwingine ana asili ya uasi na giza wanahudumuje pamoja katika asili zao kwa Mungu mmoja wa kweli? Uasi una kitu gani cha kumpa Mungu na watu wake? Giza lina kitu gani cha kumpa Mungu na watu wake? Ni kitu ambacho si sawa kabisa.

    Asiyeamini hana sehemu yo yote madhabahuni pamoja na anayeamini:
    Asiyeamini anawezaje kupokea pamoja na anayeamini kutoka kwa Mungu na kusababisha matokeo ya ki-Mungu katika ulimwengu wa roho yatakayoathili maisha ya watu? Katika ulimwengu wa roho, asiyeamini hana sehemu yo yote pamoja na anayeamini kwa sababu wapo katika falme mbili tofauti na zenye malengo mawili tofauti ambazo haziwezi kamwe kukutana. Wakati ufalme huu wa giza una lengo la kuwapeleka watu wengi iwezekanavyo Jehanamu, ufalme wa Mungu una lengo la kuwaleta watu wote kwa Yesu Kristo! Sasa, wawili wanawezaje kutembea pamoja wasipopatana? Daima hawa watu wawili hawawezi kuwa na lengo moja kwa sababu hawashiriki sehemu moja katika ulimwengu wa roho.

    Kwa sababu hizi, Biblia imetoa agizo katika ule mstari wa 17 kwamba, "Tokeni kati yao, Mkatengwe nao..." kwa lugha nyingine imepiga marufuku ushirika wo wote usio sawa (wa kiibada) na watu wasioamini hii ni pamoja na collabo kati ya mwimbaji wa nyimbo za Injili na mwimbaji wa nyimbo za kidunia. Biblia imesema, "Usiguse..." ili uwe salama na Mungu aendelee kuwa Baba kwako na wewe kwake mwana (2 Wakorintho 6:18), basi usiguse kabisa.

    Mungu akubariki sana.

    Na,

    Mch. Ezekiel P. Bundala
    0673 184 468
    0693 212 044
    0752 184 464

    #Kolabo, #Collaboration
     
    Last edited: Feb 19, 2019
    Eligibo and Tulinagwe like this.
  2. Jimmy Bunga

    Jimmy Bunga Mshirika

    Messages:
    2
    Likes Received:
    0
    Trophy Points:
    1
    Location:
    Morogoro
  3. ayubu

    ayubu Mshirika

    Messages:
    2
    Likes Received:
    0
    Trophy Points:
    1
    Location:
    tanzania
    Amina
     

Share This Page