Sehemu ya 5 IMANI NI NINI? TARAJA KATIKA IMANI

Discussion in 'Mafundisho ya Biblia' started by Ezekiel P Bundala, Aug 14, 2018.

 1. Ezekiel P Bundala

  Ezekiel P Bundala Unaishi kwa ajili ya Mungu na si kwa ajili yako

  Messages:
  657
  Likes Received:
  215
  Trophy Points:
  43
  Occupation:
  Pastor
  Location:
  Dodoma
  Waebrania 11:1

  Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.

  Imani haiwezi kuwa imani kama hakuna taraja juu ya jambo fulani au mambo fulani. Lazima kuwepo na jambo au mambo ambayo unatarajia, na mambo haya lazima uwe na uhakika nayo kabisa kwamba ni mambo halisi na yatatokea kama unavyotarajia. Kama hakuna taraja, basi, hakuna haja ya imani; na sisi tuna imani kwa sababu tunalo taraja, tunatarajia ahadi za Mungu alizotuahidi kupitia Yesu Kristo maishani mwetu na kubwa zaidi ya yote ni kukamilishwa kwa wokovu wetu siku ambayo Kristo atatufufua na kuwa pamoja naye katika uzima wa milele. Kwa hiyo mtu asiyekuwa na taraja bila shaka huyu hana imani kabisa.

  Taraja (taraji) ni nini?

  Taraja ni hali ya kutazamia au kuamania jambo fulani ya kwamba litatokea au litakuwa. Taraja linahusiana na mambo halisi yasiyoonekana ambayo kwa namna moja au nyingine mtu anayatazamia na kwa sababu hiyo anayasubiri. Kwa hiyo taraja linahusisha tumanini na saburi; hivyo, mtu anayetarajia ni mtu anayetumaini na kusubiri kile anachokitarajia, na hii haiwezekani kama mtu hana imani.

  Warumi 8:24, 25
  [24] Kwa maana tuliokolewa kwa taraja; lakini kitu kilichotarajiwa kikionekana, hakuna taraja tena. Kwa maana ni nani anayekitarajia kile akionacho?

  [25] Bali tukikitarajia kitu tusichokiona, twakingoja kwa saburi.

  Kwa nini tunahitaji kuwa na imani? Kwa sababu tumeokolewa kwa taraja na kwa sababu hiyo wokovu ni tarajio linalotimilika kila siku maishani mwetu tangu siku ya kwanza kabisa tunayookoka na tarajio hilo litakwisha siku ambayo Yesu Kristo atatutwaa na kwenda naye mbinguni. Tarajio ni kitu kinachotumainiwa kupatikana. Kwa hiyo, pasipo imani mtu hawezi kuokoka kwa sababu wokovu ni kwa taraja.

  Kama nilivyokwisha tangulia kusema ya kwamba, taraja halihusiani kabisa na mambo yanayoonekana tayari, taraja linahusiana na mambo yasiyoonekana, mambo yajayo yaliyo ya kweli yenye ushahidi na uthibitisho tulionao sasa ndani yetu unaotupa hakika ya utimilifu wa hayo tunayoyatarajia. Na kwa sababu hiyo, ndiyo sababu tunatumaini na kungoja kwa saburi utimilifu wa mambo hayo yajayo.

  Kwa lugha rahisi imani ni kuona sasa kwa hakika mambo yajayo, kisha kutarajia kwamba yatatokea na kwa sababu hiyo tunayangoja kwa saburi. Kinyume cha hapo ni kwamba, mtu hana imani, na kwa sababu hana imani, hana taraja lo lote katika maisha yake, na kwa sababu hana taraja, pia amekosa tumaini na hivyo hana cha kusubiri kinachompa tumaini la maisha mapya katika ulimwengu huu na ule ujao.

  Luka 2:25-32
  [25] Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake

  (Huyu mtu alikuwa nabii na kuhani wa Mungu, maandiko yanaonyesha kuwa alikuwa akiitarajia faraja ya Israeli; hii inaonyesha kuwa kuna kitu alikuwa anakijua katika ufahamu wake wa ndani juu ya ujio wa Masiha atakayewapa faraja Israeli. Ufahamu ule wa maandiko ndio uliompa hakika, na kwa sababu hiyo akawa anatarajia. Mbali na ufahamu juu ya maandiko, Roho Mtakatifu anatajwa kuwa juu yake, na hii ni kwa ajili ya nini? Ni kwa ajili ya kumpa hakika ya kile maandiko yanasema juu ya ujio wa Masiha; kwa hiyo mtu huyu alikuwa na imani na ndiyo maana alitarajia, na kwa sababu alitarajia, alisubiri kuona utimilifu wa ahadi hiyo.)

  [26] Naye alikuwa ameonywa na Roho Mtakatifu ya kwamba hataona mauti kabla ya kumwona Kristo wa Bwana.

  [27] Basi akaja hekaluni ameongozwa na Roho; na wale wazazi walipomleta mtoto Yesu ndani, ili wafanye kama ilivyokuwa desturi ya sheria,

  [28] yeye mwenyewe alimpokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu akisema,

  [29] Sasa, Bwana wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema;

  [30] Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,

  [31] Uliouweka tayari machoni pa watu wote;

  [32] Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli.

  Unaposoma haya maandiko, unagundua kabisa kwamba, Simeoni kwa kuyasoma maandiko ya Torati ya Musa na Manabii ambayo yanatabiri ujio wa Yesu Kristo, mtu huyu alifahamu kwa hakika juu ya ahadi hii, na kwa sababu hiyo akaanza kuitarajia. Na kwa sababu aliitarajia, Mungu alimwacha hai ili asife kabla hajaiona ahadi hii ikitimia. Na baada ya kumwona Yesu, Simeoni alikuwa tayari kufa kwa sababu hakuwa tena na kitu cha kutarajia kwa kuwa alichokuwa anakitarajia alikuwa tayari amekwisha kukiona.

  Lakini swali kubwa hapa la kujiuli ni kwamba, alijuaje kuwa yule ndiye mtoto Yesu na ndiye wokovu wa Mataifa na Israeli? Ni kwa sababu Roho Mtakatifu alikuwa juu yake ili apate kumshuhudia Yesu Kristo. Kwa Roho Mtakatifu manabii walitabiri habari za ujio wa Yesu Kristo, na kwa Roho Mtakatifu Simeoni anamwona Yesu, anaona utimilifu wa ahadi iliyoahidiwa na Mungu na kutabiriwa na manabii wake; hii ndiyo imani hasa.

  Imani inapambanua mambo kutokea kwenye uthibitisho na ushahidi wa mambo kwa Roho Mtakatifu; imani daima haimuachi mtu njia pamba, inamuelekeza na kumwongoza mtu mpaka kwenye kitu halisi kilichotangulia kunenwa. Imani haina shaka hata kidogo, ni hakika ya mambo yatarajiwayo na bayana ya mambo yasiyoonekana.

  Hatutahitaji tena imani baada ya kufika mbinguni kwa sababu taraja letu litakuwa limeishaonekana. Kwa sababu, kilichotarajiwa kikishaonekana hakuna tena haja ya kuwa na taraja; kwa hiyo imani ni kwa ajili ya mambo yale yasiyoonekana ambayo tunayatarajia, yaani mambo yajayo ambayo Mungu ametuahidi watoto wake.

  Kutarajia Yasiyoweza Kutarajiwa.
  Imani inahusisha kutarajia mambo yasiyoweza kutarajiwa, haihusishi mambo ambayo yanaweza kutarajiwa, mambo ambayo yapo katika uwezo wa mwanadamu kuyafanya na kuyatimiza; imani ni kwa ajili ya yasiyowezekana kwa wanadamu.

  Warumi 4:17 – 21
  [17] (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi) mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.

  [18] Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakuwa uzao wako.

  [19] Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa la tumbo lake Sara.

  [20] Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu;

  [21] huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi.

  Mungu alimuahidi Ibrahimu ya kuwa amemuweka kuwa baba wa mataifa mengi, lakini muda ulisonga mpaka akawa mtu mzee wa miaka miamoja asiyeweza tena kwa asili ya kawaida kusababisha ujauzito kwa mwanamke. Lakini pia kwa upande wa mke wake, Biblia inatuambia naye alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake; mbali na kuwa tasa alikuwa pia amefikia umri ambapo asingeweza kutunga mimba kwa sababu mwili wake ulikuwa umekufa (umezeeka).

  Katika mazingira haya, Ibrahimu akiiangalia ile ahadi, alitarajia ahadi hiyo ya Mungu isiyowezekana kwa asili ya mwanadamu kuwa ni kitu kinachowezekana kwa Mungu kwa sababu Mungu ni Mungu mwenye kuwahuisha wafu, na ayatajaye mambo yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako, na tena aweza kufanya yale aliyoahidi. Badala ya Ibrahimu kusita kwa kutokuamini, yeye alitiwa nguvu kwa imani, akaisubiri ahadi ya Mungu.

  Ibrahimu aliamini kama ilivyonenwa na Mungu huku akiwa anafahamu kabisa nafsini mwake kuwa Mungu ni Mungu awahuishaye waliokufa miili yao, ayatajaye mambo yasiyokuwako (ambayo hayawezekani kwa akili na uwezo au asili ya wanadamu) kana kwamba yamekuwako (yawezekane kwa nguvu zake Mungu), na kwa sababu hiyo, ni Mungu awezaye kufanya yale aliyoahidi.

  Imani ya Ibrahimu haikuwa dhana, ilikuwa ni jambo ambalo msingi wake ulikuwa katika Neno la Mungu alilolisema huku ufahamu wake ukimjua na kumfahamu huyo Mungu ni wa namna gani, na ndiyo sababu hakusita kwa kutokuamini kwa sababu alikuwa na uthibitisho na ushahidi wa kile anachokitarajia. Ijapokuwa hali ya mwili wake na mke wake pamoja na mazingira yote yalimwambia kuwa haiwezekani, imani ilimtia nguvu na kumfanya atarajie yale yasiyoweza kutarajiwa katika asili ya dunia hii.

  Ili upate kuwa vile ambavyo Mungu ametaka uwe ni lazima uamini kwa kutarajia yale yasiyoweza kutarajiwa huku ukijua hakika kwamba Mungu aweza kufanya yale yote aliyoahidi. Haiwezekani ukawa na imani usiwe na taraja juu ya utimilifu wa mambo yale yasiyowezekana. Hata wokovu wetu ni jambo lisilowezekana kwa asili ya wanadamu, na ndiyo sababu wengi watakuambia kuwa, mtu hawezi kuokoka angali yupo duniani.

  Imani yako ni mbele zake Mungu, na kutoka kwake unatarajia yote awezayo kufanya; imani yako si mbele za wanadamu katika yale wawezayo wao kuyafanya. Imani yako ikiwa ina misingi yake katika yale yanayowezekana kwa wanadamu, hiyo si imani tena ila dhana tu ambayo itakufanya utoe macho yako kwa Mungu na kuanza kuwaangalia wanadamu na mazingira yanayokuzunguka; utaanza kuangalia vitu vya asili binavyoonekana badala ya kumwangalia Mungu asiyeonekana awezaye kuwauisha waliokufa, na ayatajaye yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.

  Imani ni kuwa mbele za Mungu na kumwangalia Mungu huku ukitarajia wokovu kutoka kwake. Imani ni kutoka kabisa mbele za watu na katika asili ya ulimwengu huu; ni kuondoa macho yako ya ndani yasitazame asili ya wanadamu na kuyaelekeza kwa Mungu; unakuwa kipofu kwa yale yanayoonekana kwa macho ya damu na nyama, lakini unakuwa na uwezo wa kuyaona mambo ya Mungu yasiyokuweko katika asili ya kawaida bali rohoni. Huku ni kuwa mbele za Mungu na si mbele za ulimwengu huku ukitarajia utimilifu wa ahadi za Mungu. Hii inawezekana tu iwapo utazama katika Neno la Mungu, katika Yesu Kristo na katika Roho Mtakatifu, ufahamu wako ukawa na nuru ya mambo haya matatu na ukakaa katika hayo.

  Kwa hiyo, kama unataka kuwa na imani, dumisha ushirika wako na mambo haya matatu kwa sababu hayo ndiyo imani ya Ki-Mungu (God's kind faith) inayoleta matokeo; kwa hiyo kwa kadiri ufahamu wako unavyokua katika kumjua Yesu Kristo, na Neno lake, na Roho Mtakatifu na kuwa na ushirika nao wote watatu, ndivyo unavyokuwa imara katika imani, na ndipo kwako hakutakuwa na jambo lisilowezekana. Kwa lugha nyepesi, kuwa na imani ni kuwa mmoja na Mungu, ni kusimama na Mungu, na ni kutembea na Mungu. Hii haiwezekani mpaka umemjua.

  Mungu akubariki sana.

  Na,

  Mch. Ezekiel P. Bundala
  0673 184 468
   
  Eliudy ML YoLoGood likes this.
 2. Mashaka Mponeja

  Mashaka Mponeja Mshirika

  Messages:
  1
  Likes Received:
  0
  Trophy Points:
  1
  Location:
  Mwanza
 3. Eliudy ML YoLoGood

  Eliudy ML YoLoGood Mshirika

  Messages:
  1
  Likes Received:
  0
  Trophy Points:
  1
  Occupation:
  Mwl. wa NENO
  Location:
  Arusha
  Amina, ubarikiwe sana.
   

Share This Page