Sehemu ya Kwanza NDOA EDENI YANGU.

Discussion in 'Mahusiano, Uchumba na Ndoa' started by Ezekiel P Bundala, Oct 18, 2023.

  1. Ezekiel P Bundala

    Ezekiel P Bundala Unaishi kwa ajili ya Mungu na si kwa ajili yako

    Messages:
    657
    Likes Received:
    215
    Trophy Points:
    43
    Occupation:
    Pastor
    Location:
    Dodoma
    EDENI - BUSTANI YA MUNGU

    “BWANA Mungu akapanda bustani upande wa mashariki wa Edeni, akamweka ndani yake huyo mtu aliyemfanya.”
    ‭‭Mwa‬ ‭2‬:‭8‬ ‭


    “Maana BWANA ameufariji Sayuni; amepafariji mahali pake palipokuwa ukiwa; amefanya jangwa lake kuwa kama bustani ya Edeni, na nyika yake kama bustani ya BWANA; furaha na kicheko zitaonekana ndani yake, kushukuru, na sauti ya kuimba.”
    ‭‭Isa‬ ‭51‬:‭3‬


    “Ulikuwa ndani ya Edeni, bustani ya Mungu; kila jiwe la thamani lilikuwa kifuniko chako, akiki, na yakuti manjano, na almasi, na zabarajadi, na shohamu, na yaspi, na yakuti samawi, na zumaridi, na baharamani, na dhahabu; kazi ya matari yako na filimbi zako ilikuwa ndani yako; katika siku ya kuumbwa kwako zilitengenezwa tayari.”
    ‭‭Eze‬ ‭28‬:‭13‬ ‭


    Mungu anayo bustani, na bustani hiyo ni Edeni, mahali ambapo uwepo wake upo na kila aina ya neema ndani yake ya kumwezesha mwanadamu kuishi kama ambavyo Mungu amemkusudia aishi. Bustani ya Edeni siyo wazo la mwanadamu, ni wazo la Mungu kwa ajili ya mwanadamu. Kwa hiyo, siyo ubunifu na uumbaji wa mwanadamu, ni ubunifu na uumbaji wa Mungu. Mungu alipoiumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake siku zile za uumbaji, akiisha kumaliza kuumba dunia yote, alishuka duniani, akapanda bustani mashariki mwa Edeni, bustani yake kwa ajili ya mwanadamu, akaiwekea kila kitu kilichohitajika na mwanadamu ili aishi, kisha baada ya kukamilisha kila kitu, alimtwaa Adamu aliyekuwa tayari amemuumba akamweka ndani ya bustani hiyo ya Edeni. Kisha akamwagiza kuwa ailime na kuitunza ili iendelee kubaki katika ubora ule ule na kama ambavyo Mungu aliikusuduia.


    KUSUDI LA MUNGU KUPANDA BUSTANI YA EDENI
    Mungu alitaka mwanadamu aishi maisha ya furaha, akifurahia kila kitu katika kila siku anayoishi duniani. Moja ya jambo ambalo Mungu alitaka mwanadamu afurahie, ni uwepo wa Mungu kwa Adamu kuwa na ushirika na Mungu. Bustani ya Edeni ni mahali pa uwepo wa Mungu. Mungu alikuja kila siku kwa uwepo unaodhihirika na kuwa na mazungumzo na Adamu na Hawa. Ingawaje wakati wote alikuwepo ndani ya bustani, lakini kuna wakati (wakati wa jua kupunga), Mungu alidhihirisha uwepo wake huo hata akaonekana macho kwa macho kwa Adamu na Hawa.

    Pili, Mungu alitaka mwanadamu awe na mahali maalumu pa kuishi katika dunia, yaani, nyumbani na kuendesha maisha yake yote hapo. Kwa hiyo, Mungu alimtengenezea bustani ya Edeni iwe nyumbani, mahali ambapo Adamu ataishi na familia yake na kufurahia kila neema ambayo Mungu ameiachilia kwa ajili yake. Mungu hakutaka Adamu aishi kwenye dunia bila kuwa na makao ambayo maisha yake yote na ya familia yake yataendeshwa hapo. Alitaka Adamu awe na makao maalumu duniani ya kudumu yenye utoshelevu wa kila aina.

    Tatu, Mungu alitaka Adamu awe na mahali ambapo atafurahia uhusiano wake wa kindoa na Hawa. Bustani ya Edeni ilikuwa ni mahali pa ndoa yao, mahali ndoa inaanzia na kuendelea. Umeishawahi kujiuliza ni kwa nini Mungu hakumuumba Hawa kabla ya Yeye kupanda bustani ya Edeni? Adamu aliumbwa kabla ya Mungu kupanda bustani ya Edeni, lakini hawa aliumbwa baada ya bustani ya Edeni kupandwa. Hii ni kwa sababu Mungu alitaka uhusiano wa ndoa uanzie kwenye makao yaliyoandaliwa, mahali pa uwepo wake, mahali palipopangiliwa vyema, penye utaratibu, nyumbani kwa Adamu. Mungu alitaka bustani ya Edeni iwe mahali ambapo ndoa itaumbwa, na kufungwa.


    Niseme kidogo jambo ambalo ni kanuni ya kufuata kabla ya ndoa kisha tutaendelea na hoja yetu. Adamu aliumbwa kabla bustani haijapandwa, lakini Hawa aliumbwa baada ya bustani kupandwa na Adamu akishakuwa ndani ya bustani tayari. Hawa aliumbwa ndani ya bustani na siyo nje ya bustani, lakini Adamu aliumbwa bustani ikiwa haipo kabisa. Wazo la ndoa linakuja baada ya uwepo wa bustani ya Edeni na Adamu akiwa ndani yake. Mungu anasema kuwa, Si vema mtu huyu awe peke yake... Adamu akiwa tayari ndani ya bustani. Wakati Adamu akiwa hayupo bustanini kabla ya bustani kuwepo, Mungu hakusema cho chote kuhusu kumfanyia Adamu msaidizi. Hii maana yake ni nini? Kabla mwanaume hajawa na makao, yaani mahali pa yeye na mkewe kuishi hana uhalali wa kuoa. Hapaswi kuanzisha wazo la kuoa. Wazo la kuoa linakuja baada ya kuwepo kwa makao ambayo mwanaume huyo anaishi lakini pia uwezo wa kumudu mahitaji yote ya kimaisha. Tutaizungumzia zaidi hii katika "Muundo wa ndoa wa Mungu." Sasa tunaweza kuendelea.

    Hawa aliumbwa kutoka kwa Adamu lakini ndani ya bustani ya Edeni ambayo Mungu aliipanda na kisha akamtwaa Adamu na kumweka ndani yake. Hii ni ajabu, na ni siri kubwa. Hii maana yake ni kuwa, kwa asili, ndoa ilikusudiwa kuwa ni bustani yenye utoshelevu wa kila kitu, mahali ambapo mke na mume watafurahia, wakifurahiana kwa kuwa washirika kila mmoja kwa mwenzake wa kile Mungu amewaumba kuwa na amewaumbia kwa ajili ya matumizi yao ya kila siku. Unaposoma kitabu cha Wimbo Ulio Bora, unagundua kuwa, uhusiano wa ndoa unafananishwa na bustani. Mwandishi wa kitabu hiki anaturejesha Mwanzo katika bustani ya Edeni akielezea uzuri wa ndoa na utoshelevu wake akitumia lugha ya bustani nzuri iliyochanua.

    “Bustani iliyofungwa ni umbu langu, bibi arusi, Kijito kilichofungwa, chemchemi iliyotiwa muhuri. Machipuko yako ni bustani ya komamanga, Yenye matunda mazuri, hina na nardo, Nardo na zafarani, mchai na mdalasini, Na miti yote iletayo ubani, Manemane na udi, na kolezi kuu zote. Wewe ndiwe chemchemi ya bustani yangu, Kisima cha maji yaliyo hai, Vijito vya Lebanoni viendavyo kasi. Amka, kaskazi; nawe uje, kusi; Vumeni juu ya bustani yangu, Manukato ya bustani yatokee. Mpendwa wangu na aingie bustanini mwake, Akayale matunda yake mazuri.”
    ‭‭Wimbo‬ ‭4‬:‭12‬-‭16‬ ‭

    “Naingia bustanini mwangu, umbu langu, bibi arusi, Nachuma manemane yangu na rihani, Nala sega la asali na asali yangu, Nanywa divai yangu na maziwa. Kaleni, rafiki zangu, kanyweni, Naam, nyweni sana, wapendwa wangu.”
    ‭‭Wimbo 5‬:‭1‬

    Ndoa ikiwa bustani ya Mungu (kwa maana kama Mungu alivyopanda bustani ya Edeni, ndivyo alivyoiunganisha ndoa ndani ya bustani hiyo) imekusudiwa kuzalisha furaha kwa wanandoa siku baada ya siku. Unaposoma kifungu cha maandiko ya kitabu cha Isaya 51:3 utaona Mungu anaambatanisha wazo la bustani yake na wazo la furaha na kicheko. Ndoa ni bustani ya furaha na kicheko kwa wanandoa. Ilikusudiwa iwe Edeni, mahali pa furaha na kicheko na si mahali pa huzuni, uchungu na maumivu. Maandiko yanasema, "... furaha na kicheko zitaonekana ndani yake, kushukuru, na sauti ya kuimba." Hii maana yake ndani ya bustani ya Mungu, (katika sombo hili ni ndoa), Mungu amekusudia kwamba, katika kila siku wanayoishi wanandoa, furaha na kicheko zionekane ndani yake pamoja na kushukuru na sauti ya kuimba.

    Katika nyakati za Biblia, watu walipokuwa wamejazwa na furaha, ili kuionyesha furaha yao, waliitikia kwa kuimba nyimbo kwa furaha. Nyimbo ni ishara kwamba mtu amejazwa na furaha na shukrani. Kwa kweli, wanandoa ndani ya bustani yao wanapaswa kusikika wakiimba nyimbo za furaha, yaani, wakitaja matendo mazuri wao kwa wao mara zote wanayofanyiana na yale Mungu anayowatendea. Furaha na kicheko, shukrani na sauti ya kuimba ni sifa ya ndoa ikiwa kama bustani ya Edeni. Wanandoa wafurahie, wacheke, washukuru na kuimba pamoja badala ya kulia, kuhuzunika, kulaumu au kulalamika na kuomboleza. Hii inawezekana iwapo kila mmoja amejitoa kwa Mungu, na kujitoa kwa mwenziwe akifanya kila jambo kwa utukufu wa Mungu na kwa ajili ya furaha ya mwenzi wake wa ndoa.

    SHETANI NDANI YA BUSTANI YA EDENI.
    Ukweli kwamba bustani ya Edeni ilipandwa na Mungu na kutawaliwa pande zote na uwepo wa Mungu haikumzuia Shetani kuingia bustanini na kuwajaribu Adamu na Hawa. Pamoja na Mungu kuipanda bustani ya Edeni, kuijaza kwa uwepo wake, na Yeye mwenyewe kudhihirika katika ibada ambayo wanandoa hawa waliifanya pamoja kila siku wakati wa jua kupunga, bado haikumzuia Shetani kuingia bustanini na kuwajaribu. Ukweli kuwa ndoa imeunganishwa na Mungu, inamejaa uwepo wa Mungu, na Mungu anadhihirika kila wanandoa wanapomfanyia Mungu ibada na kuomba, haimzuii Shetani kuja katikati ya ndoa yao na kuwajaribu ili kuivuruga au kuiharibu ndoa yao. Shetani atakuja na kuwajaribu, na Mungu kamwe hatamzuia Shetani asiwajaribu wanandoa. Ila wanandoa wanapaswa wajilinde na Shetani asiwaguse, na badala yake wamkaribie Mungu na kumpinga Shetani naye atawakimbia.

    Ni muhimu wanandoa wakafahamu na kuelewa jambo hili, kuwa, Shetani atakuja katikati kabisa ya ndoa yao, na siyo pembezoni mwa ndoa yao na kuwajaribu kama ambavyo aliingia ndani ya bustani na kwenda katikati kabisa ya bustani mahali ambapo mti wa uzima na mti wa ujuzi wa mema na mabaya ilipandwa na Mungu. Kwa hiyo, mkiwa wanandoa ndani ya ndoa yenu ambayo ni bustani yenu ya Edeni, tarajieni kabisa ujio wa ugeni wa Shetani, na yeye kila anapokuja, huwa haji na kukaa pembeni pembeni mwa bustani, huja na kukaa katikati ya bustani ili aibe, aharibu na kuchinja (kuua). Na katika kutekeleza kazi yake hii hutumia udanganyifu au uongo. Kwa hiyo wanandoa watamshinda iwapo tu watakuwa wanajua kwa hakika ukweli wa mapenzi ya Mungu na kuchagua kuutenda.

    Shetani akija ili kuiba, kuharibu na kuchinja, haji na kuanza kuzungukia pembeni pembeni, huja na kutulia katikati katika mawazo ya wanandoa, mahali pa ujuzi wa mema na mabaya na mahali pa uzima. Huanza kuwajaribu wanandoa katika muktadha wa wao kukoseana na kumkosea Mungu. Wanandoa ikiwa hawatazijua njama za Shetani na mpango wake wa kuiba, kuharibu na kuua furaha yao na pengine ndoa yao, wataingia kwenye mtego wa Shetani na kisha kuumia. Katika hili, wanandoa wanapaswa wawe wenye hekima na busara, wakizijua njama za Shetani, na kisha kumpinga kila inapohitajika kufanya hivyo, lakini pia kujiepusha na kila njia yake inayoweza kuwaelekeza kwenye ubaya.

    “Mwenye busara huyaona mabaya na kujificha; Bali wajinga huendelea mbele wakaumia.”
    ‭‭Mithali ‬ ‭22‬:‭3‬

    KUILIMA NA KUITUNZA BUSTANI
    Kupewa bustani siyo jambo gumu. Ugumu unakuja kwenye kuilima na kuitunza. Kuilima bustani ni kuifanyia kazi ili iendelee kuchipusha kila kinachohitajika ndani yake; ni kuivika au kuivalisha bustani kupitia kuchipusha, kukuza na kuzalisha mimea au miche inayokidhi kila uhitaji wa mwanadamu na kuifanya ionekane ya kupendeza. Hii inahusikana na namna unavyoshughulika na ardhi. Kutunza ni kuilinda na kuichunga kwa kuwa na tahadhari na hadhari yote ili iwe salama. Ni kuchukua tahadhari na kuwa na hadhari wakati wote ili asije mtu akasababisha uharibifu kwa kutumia hila. Hii haihusiani na jinsi unavyoshughulika na ardhi, inahusika na namna unavyohusika na akili na ufahamu wako wa moyoni katika kutambua mapenzi ya Mungu na au dhidi ya hila au udanganyifu wa Shetani. Wakati kuilima (kuifanya ipendeze, ichipushe kila kitu chema kinachohitajika) inahusikana na wewe kushughulika na ardhi, yaani ndoa yenyewe, kwa kufanya kila kinachohitajika ili isiwe isiyozaa matunda; kuitunza inahusikana na kuilinda au kuichunga ndoa yako kwa kujilinda mwenyewe ufahamu wako na moyo wako dhidi ya udanganyifu wa Shetani. Unaweza kuifanya izae matunda lakini ukaipoteza!

    Adamu alipewa bustani, aliweza kuilima, lakini alishindwa kuitunza. Ndivyo ilivyo kwa ndoa nyingi; wengi wanapewa waume au wake, wanaweza kufanya majukumu yao kuhakikisha ndoa inaonekana ya kupendeza, lakini wanashindwa kuzitunza ndoa zao. Kwa sababu gani? Kwa sababu inapokuja suala la kuitunza ndoa inayohitajika hapo ni mambo mawili, kuyajua mapenzi ya Mungu na kuyatii, na mbili kuzijua hila za Shetani, kuzikataa na kumpinga kwa neno la Mungu. Nitakupatia mifano mitatu tu katika Biblia.

    Yesu Kristo alibatizwa, alijazwa Roho Mtakatifu, na alifunga siku arobaini mchana na usiku bila kula. Hapo aliweza kuilima bustani yake ambayo ilikuwa ni huduma yake. Mwisho wa siku arobaini alipoona njaa, Shetani alikuja kumjaribu. Yesu aliyajua mapenzi ya Mungu, akayatii, na pia alijua hila na udanganyifu wa Shetani na kwa sababu hiyo alitumia Neno la Mungu kumpinga Shetani. Hapa Yesu hakutumia ubatizo, wala mfungo, wala ujazo wa Roho Mtakatifu kumpinga Shetani, bali alitumia Neno la Mungu lililoujaza ufahamu wake na akili zake za moyoni. Unaweza kuilima bustani lakini ukashindwa kuitunza. Yesu aliweza vyote, kuilima na kuitunza. Maombi, mfungo, kuongozwa na Roho, kumtumikia Mungu, na kusoma Neno la Mungu hakumzuii Shetani, ambaye ni mjaribu kuja kwako, ndani ya ndoa yenu na kukujaribu. Kwa hakika atakuja tu! Ni muhimu pia ukaelewa kuwa kila kilicho chema, kilichofanywa na Mungu, humvutia Shetani aje ili akiibe, akiharibu na akichinje. Kwa hiyo, wewe unapaswa ukitunze.

    Mfano wa pili ni ule wa mfalme Sauli. Sauli anapewa ufalme na Mungu. Anapata mafanikio, anaufanya ufalme kuwa na matunda. Anawashinda maadui wa Israeli na wa Mungu. Ufalme unastawi na kuongezeka. Lakini anashindwa kuutunza ufalme ule na hatimaye anaupoteza. Mfalme Sauli anashindwa kumtii Mungu, anadanganyika na kufanya mapenzi yake mwenyewe na ya watu dhidi ya mapenzi ya Mungu; badala ya kumuogopa Mungu anawaogopa watu. Labda ni kweli alikuwa na nia ya kumtolea Mungu sadaka za kuteketezwa, ndiyo sababu alihifadhi wanyama wanono, lakini kwa wakati huo kutoa sadaka haikuwa mapenzi ya Mungu makamilifu, bali kutii maagizo ya Mungu. Kutokutii kwake kulimfanya apoteze ufalme. Udanganyifu wa mali unaotokana na tamaa ya mali uliudanganya moyo wa mfalme Sauli, na kwa hiyo akashindwa kuutunza ufalme.

    Mfano wa tatu wa maandiko ni ule unaotoka katika kitabu cha Yakobo 4:7 ambapo Yakobo anasema kuwa, Basi mtiini Mungu, mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Anaanza na kumtii Mungu kabla ya kumpinga Shetani. Kumtii Mungu kunatanguliwa na kuyajua mapenzi ya Mungu ambayo ni Neno lake. Tukiyajua na tukayatii, tutazijua hila za Shetani, na kwa hiyo hatimaye, atakapokuja tutampinga, naye atatukimbia kabisa. Na hapo ndipo tutakapokuwa tumeweza kuitunza bustani.

    Haijalishi tunafanya mambo gani mazuri ili kuboresha na kupendezesha ndoa zetu, kama hatutajua mapenzi ya Mungu katika ndoa zetu na kuyatenda, tutapoteza ndoa za kiungu zenye furaha na kubakiwa na ndoa za kipagani nje ya Edeni, ambayo tutakuwa mbali na uwepo wa Mungu, na miiba na michongoma itakuwa ni mahali pa ndoa zetu. Suala siyo tu kuwa na ndoa nzuri au bora, bali pia ni kuwa na uwezo wa kuilima na zaidi kuliko yote kuitunza kwa kumtii Mungu katika mapenzi yake yote, yaani, Neno lake.

    Ndoa ni bustani ya Mungu kwa ajili ya wanandoa ili waishi maisha ya furaha, kicheko, shukrani na sauti ya kuimba kwa sababu ya utoshelevu wa maisha, wanaoupata kutoka katika uwepo wa Mungu ndani ya bustani hiyo katika kila eneo la maisha yao. Kwa hiyo, wanandoa hawa wanalo jukumu la pamoja kama washirika pamoja na Mungu kila mmoja kwa mwenziwe la kuilima na kuitunza ndoa yao ili iendelee kuwa katika hali ambayo Mungu aliikusudia na kuifanya iwepo na iendelee kuwazalishia furaha na kicheko, shukrani na sauti ya kuimba. Ni matumaini yangu, wewe pamoja na mwenzi wako wa ndoa mtaifurahia hii bustani yenu mliyopewa na Mungu iwe mahali penu pa furaha, kicheko, shukrani na sauti ya kuimba; mahali ambapo kila kitu kinachanua na kutoa harufu nzuri ya kupendeza na kufurahiwa na wote wawili, mume na mke.

    Na,

    Mch. Ezekiel Paul Bundala
    +255 673 184 468
     

Share This Page